Jumanne 16 Juni 2026 - 00:30
Baraza la Wanazuoni wa Kishia Afghanistan Lasisitiza Umuhimu wa Kuhakikishwa Usalama Kwenye Maadhimisho ya Maombolezo ya Muharram Nchini Humo

Hawza/ Sambamba na kuwadia mwezi wa Muharram, Baraza la Wanazuoni wa Kishia Afghanistan limetoa taarifa likisisitiza umuhimu wa kuandaliwa kwa maadhimisho ya maombolezo kwa utukufu, utulivu na usalama, na kuwataka maafisa wa usalama nchini humo kuhakikisha usalama wa maadhimisho hayo na kulinda haki za kidini na kimadhehebu za wananchi.

Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Hawza, katika taarifa hiyo iliyotolewa leo Jumatatu tarehe 25 Khordad 1405 Shamsia, (15 June 2026) kwa kunukuu Hadithi ya Mtume (saww):

«حُسَینٌ مِنّی وَ أَنَا مِنْ حُسَین»

(Hussein ni sehemu yangu na mimi ni sehemu ya Hussein),

Mapinduzi ya Ashura yameelezwa kuwa ni madrasah ya heshima, uhuru, kutetea uadilifu, kuamrisha mema, kukataza maovu na kusimama dhidi ya dhulma na ufisadi.

Baraza la Wanazuoni wa Kishia Afghanistan, limebainisha kwamba; harakati ya Hadhrat Imam Hussein (as) ni taa inayowaongoza watu huru wa dunia na ni chanzo cha hamasa kwa mataifa yaliyodhulumiwa katika kipindi chote cha historia.

Baraza hilo limewaomba Waumini wote na waandaaji wa maadhimisho ya maombolezo kwamba, kama ilivyokuwa katika miaka iliyopita, waendeshe ibada na shughuli za Ashura kwa hamasa na utambuzi wa Husseini, bila ya kuwepo vizuizi vyovyote.

Katika sehemu nyingine ya taarifa hiyo, limesisitiza umuhimu wa kufafanua kwa usahihi malengo na ujumbe wa Ashura, na limewataka makhatibu, wahubiri na wasomaji wa masaibu kuwafahamisha vijana kwa umakini na uwajibikaji kuhusu dhana kama vile kutetea uadilifu, kuwajibika na kulinda maadili ya Kiislamu.

Baraza la Wanazuoni wa Kishia Afghanistan pia limewaomba wahadhiri na waandaaji wa maadhimisho kujiepusha na kuwasilisha maudhui yoyote ambayo yanaweza kusababisha mifarakano na mgawanyiko miongoni mwa Waislamu wa nchi hiyo.

Katika taarifa hiyo, kuhifadhi umoja, kuimarisha mshikamano wa kijamii na kujiepusha na kauli zozote zinazoweza kuibua mivutano katika mazingira ya kidini na kijamii, kumetajwa kuwa miongoni mwa mambo muhimu yanayopaswa kuzingatiwa katika siku za Muharram.

Aidha, viongozi wa misafara na vikundi vya maombolezo wameombwa kushirikiana kikamilifu na maafisa pamoja na vikosi vya usalama ili maadhimisho ya Muharram na Ashura yafanyike katika mazingira ya utulivu, usalama na mbali na aina yoyote ya vitisho.

Wakati huohuo, Baraza la Wanazuoni wa Kishia Afghanistan limezitaka taasisi zinazohusika na usalama kuchukua hatua na maandalizi yanayohitajika ili kuwezesha kufanyika kwa maadhimisho hayo kwa utukufu na usalama katika maeneo yote ya nchi, na kuzingatia haki za kidini na kimadhehebu za wananchi wote.

Katika sehemu ya mwisho ya ujumbe wake, baraza hilo limewahutubia pia wafadhili na watu wanaotoa nadhiri, likiwaomba kuzitilia maanani zaidi familia zisizojiweza na wahitaji, hususan wahamiaji, wakati wa kugawa sadaka, misaada na nadhiri mbalimbali.

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha